Na: Mwl; Samwel Mkumbo.
Hakika Baraka ni jambo mojawapo la msingi sana kwa watoto wa Mungu na ni jambo la Faraja tuonapo mwana wa Mungu akifanikiwa katika mambo yake yote. Kama inenwavyo;

..,….Mzee, kwa Gayo mpenzi, nimpendaye katika kweli. Mpenzi naomba ufanikiwe katika mambo yote na kuwa na afya yako, kama vile roho yako ifanikiwavyo…,… (3Yoh 1:1-2)

Sasa basi ni vema ukafahamu  ya kuwa kubarikiwa ni jambo la msingi sana na tena ni moja ya ushuhuda kwa watoto wa Mungu. Lakini pia Baraka ni kutukuka sana katika Ukuu wa Mungu na pia juu ya haya yote tunaweza kuona ni kwa jinsi gani uweza  wa Mungu unajidhihirisha katika mambo yetu ya mwilini naam katika kutuma mema katika Tumaini jipya la imani yetu.

Lakini pia Biblia inatupa maelezo kadhaa juu ya kupata Baraka au mafanikio maana si kila mafanikio (Baraka) zina mkono wa Mungu ndani yake, au ni utukufu wa Mungu mingine ni mitego ya shetani katika kutuangusha katika imani yetu katika KRISTO YESU, naam! Maandiko matakatifu yanatupa mifano kadhaa ya Baraka zitokazo kwa Mungu na ziletwazo na mwovu kama mtego kwetu.

Vielelezo!!

-Habari za Elisha na Naamani.

2 Wafalme 5:1-14 tunaona kisa kizuri na cha kutufundisha juu ya Baraka.

Nabii Elisha alipata nafasi ya kufanya muujiza wa uponyaji kwa Naamani (Yule jemadari wa Shamu) juu ya ukoma wake, na baada ya muujiza huo, mtu huyo, huyo Naamani alitaka kumpa zawadi Elisha, lakini Elisha hakukubali,. 2 Wafalme 5: 15-16 inasema;

Akamrudia Yule mtu wa Mungu, yeye na mafuatano yake yote. Akaja, akasimama mbele yake; akasema, Sasa  tazama, najua ya kwamba hakuna Mungu duniani mwote, ila katika Israeli; basi nakuomba upokee mbaraka kwa mtumwa wako. Lakini akasema, Kama BWANA aishivyo ambaye nimesimama mbele yake, sipokei kitu. Akamshurutisha apokee, lakini akakataa.

Katika maandiko hayo utaona ya kuwa Elisha hakupokea Baraka kutoka kwa Yule Jemadari naam, huyo  Naamani, lakini ni vema tukafahamu ya kuwa si kwa sababu Elisha alikuwa na tabia ya kutopokea zawadi na Mbaraka kutoka kwa watu aliowahudumia, la hasha! Bali ipo sababu nyingine, maana  ni Elisha huyu huyu alipokea msaada kutoka kwa mama Mshunami! Tazama hapa;  2Wafalme 4:8

Kwa hiyo si kila tunuku unayopewa ni ya kukubali lakini pia si zote ni za kukataa maana kila jambo lina maana yake na matokeo yake ambayo kwa hayo twaweza kutambua kusudi na mapenzi ya Mungu kwetu lakini pia hila na mitego ya shetani.



-Mfano wa Yesu.

Moja ya mifano tunayoweza kupata kuhusu habari ya Baraka au kutunzwa ni kuhusu habari za Yesu mwenyewe. Luka 4:5-7 imeandikwa hivi;

Akampandisha juu, akamwonyesha milki zote za ulimwengu kwa dakika moja. Ibilisi akamwambia, Nitakupa wewe enzi hii yote, na fahari yake, kwa kuwa imo mikononi mwangu, nami humpa ye yote kama nipendavyo. Basi, wewe ukisujudu mbele yangu yote yatakuwa yako.

Katika mistari hiyo unaweza kuona mfano wa Baraka ambazo huja kwetu kama mtego, maana katika kutazama hayo waweza kuona namna ambavyo shetani aweza kufanya aina flani ya mafanikio kwetu na huja kwa mtindo wa kututamanisha sana hata kutuvuta karibu nazo  lakini kumbe ni njia ya upotevu.

NAMNA YA KUTAZAMA BARAKA/MAFANIKIO YANAYOKUJIA YANATOKA WAPI.

Katika nafasi tupate kujua japo kidogo namna ya kutazama Baraka na mafanikio yetu na yanayotujia kuwa yanatoka wapi ili iwe ni nafasi nzuri kwetu kujua ni kwa jinsi gani tutamtukuza Mungu kwa anavyotuwezesha au ni kwa jinsi gani tunaweza kukwepa mishale ya mwovu anayoturushia kwakutumia kifuniko cha Baraka au mafanikio.

Ø  Lengo la Anayetoa.

Kutambua lengo la anayetoa sadaka ni njia mojawapo ya kujua ni chanzo gani hizo Baraka au mafanikio yanabubujika, maana kila sadaka au kitu unachopokea au anachokupatia mtu kina lengo lake, kwa hiyo kutazama nini lengo ni njia mojawapo inayoweza kusaidia.





Vielelezo.

·         Kuhusu Yesu.

Ukitazama vizuri habari za Yesu hapo juu unaweza  kugundua nini lilikuwa lengo la shetani kutaka kumtunuku mtu au kutoa kitu, tazama alivyomwambia Yesu;

…….. Nitakupa wewe enzi hii yote, na fahari yake, kwa kuwa imo mikononi mwangu,……..,,. Basi, wewe ukisujudu mbele yangu yote yatakuwa yako..,...(Luka 4:5-7). Sasa unaweza kugundua kuwa si kwamba Yesu hakuhitaji hizo fahari ila nini lengo la shetani kumpa,.. tazama tena alivyosema…….. Basi, wewe ukisujudu mbele yangu yote yatakuwa yako..,..

Maana Yesu alikuwa ni muhitaji wa mambo ya mwilini pia yaani chakula, mavazi na malazi, ndio! Alihitaji hayo pia na kuna watu  walimhudumia katika hayo na hakukataa, maana imeandikwa hivi katika Injili ya Luka;

Na wanawake kadhaa wa kadhaa ambao walikuwa na pepo wabaya na magonjwa wakaponywa;……..na wengine wengi, waliokuwa wakimhudumia kwa mali zao.(Luka 8:2)

Yesu hakukataa kwa wanawake na watu hao kumhudumia kwa mali zao lakini alikataa kupewa Milki na fahari ya Ulimwengu na shetani (kwa kumsujudia), nini sababu? Bila shaka ni LENGO!!

Ø  Chanzo cha Mapato ya Anayetoa/ Chanzo cha Sadaka yenyewe.

Kuna wakati tunaweza kujua nini uamuzi wa kufanya au nini ni nia ya sadaka tunayopokea kwa kuangalia chanzo cha mapato ya anayetoa, au chanzo cha sadaka hiyo. Tazama mfano huu;

Huyo mfalme akawaagizia posho ya chakula cha mfalme,na ya  divai aliyokunywa, akaagiza walishwe hivyo muda wa miaka mitatu; ili kwamba hatimaye wasimame mbele ya mfalme……….. Lakini Danieli aliazimu moyoni mwake ya kuwa hatajitia unajisi kwa chakula cha mfalme, wala kwa divai aliyokunywa…….. (Danieli 1: 5, 8).

Ninachotaka tuone hapo ni kwamba pamoja ya kwamba hawa vijana watatu, naam, huyo Danieli, Meshaki, Shedraki na Abednego walipata nafasi ya kupata chakula kizuri kutoka katika meza ya mfalme tena wakiwa katika nchi ya ugeni bila kusahau walikuwa na hadhi ya utumwa, lakini hawakukubali kupokea hiyo Baraka au zawadi kutoka Ikulu, tena Biblia imeweka kweupe sababu yao, ni kwamba hawakutaka kujitia unajisi.

Maana walijua ya kuwa kuna uwezekano ya kuwa kama  ni nyama basi zitakuwa zilizokuwa zimetolewa sadaka kwa miungu ya Wababeli, lakini pia hawakupenda kunywa mvinyo yao wala kitu chochote, lakini pia hawakutaka kujitia unajisi kwa chakula cha mfalme na ilikuwa ni mila na desturi ya wayahudi kutoshiriki chakula na watu wa mataifa.

Japokuwa biblia haijaweka kweupe ni lini hasa au wakati ambao hao wakina Danieli waliacha kula mtama au ni lini walianza kula vyakula vya kawaida lakini sabab kubwa ya kukataa ni kwamba walikataa chanzo cha chakula hicho.

Ø  Uhusiano wa mtoaji na watu wengine.

Kuna wakati mwingine watu hupenda kuwafadhili watumishi wa Mungu na kuonesha wema kwa watumishi wa Mungu, tena sana. Lakini unakuta mtu huyo huyo huwatendea watu wa nyumbani mwake mambo maovu, na hata kama si watu wa nyumbani mwake lakini hata watu wengine wa kawaida huwatendea mambo yasiyo mema wala hawafadhili, au kuwatendea wema nga kidogo. Jambo kama hilo si jema na ni vema mtu kama huyo uwe nae makini sana maana inaweza kuwa mtego sana kwako, lakini pia inaweza kuwa laumu kwa hao anawatendea mabaya maana wanaweza kuona kuwa unawafanyia fitina,. Tusome pamoja hapa; 

……..Kwa hiyo kadiri tupatavyo nafasi na tuwatendee watu wote mema; na hasa jamaa ya waaminio….(Wagalatia 6:10).

Lakini kwa makini tena tazama maneno haya…………tuwatendee watu wote mema;….na hasa jamaa ya waaminio…..



Ushauri wa Ziada.

Katika kukaa katika nafasi nzuri ya utumishi na mahusiano mazuri na watu na namna ya kuangalia jinsi tunavyotumika tazama kitabu cha TIMOTHEO.

chanzo upanga wa roho blog.