Jambo la kwanza
Kuoa au kuolewa kunabadilisha uhusiano
wako na wazazi wako.
Mwanzo.2:24 anasema, “Kwa hiyo mwanamume atamwacha baba yake na mama yake naye ataambatana na mkewe, nao watakuwa mwili moja”. Ukiangalia (Zaburi.45:10-11) anasema, “Sikia binti utazame (maana yake anazungumza na msichana) utege sikio lako. Uwasahau watu wako na nyumba ya baba yako na mfalme atautamani uzuri wako, maana ndiye bwana wako naye umsujudie”.
Najua watu wengi sana wanataka waingie kwenye ndoa, waoe au waolewe, lakini uhusiano wao na wazazi wao usibadilike, haiwezekani. Biblia imeweka wazi kabisa, unataka kuoa, mwanamume lazima kwanza aachane na baba yake na mama yake, maana yake kuna mabadiliko. Kuna mabadiliko mahali pakuishi, kuna mabadiliko juu ya mtazamo wako wa kwanza wa maisha yako. Mke wako hawezi kuwa mama yako, na mume wako hawezi kuwa baba yako. Mke wako anakuwa mke wako na si mama yako. Mume wako anakuwa mume wako na si baba yako.
Na kabla hujafikia maamuzi ya namna hiyo - ukiingia kwenye ndoa, ndoa yako itakuwa ngumu. Maana inawezekana unaishi vizuri na wazazi wako, kiasi ambacho maamuzi yako yoyote unayofanya lazima ushirikiane nao, na hiyo ni hatua nzuri kabisa. Lakini ukiishaingia kwenye ndoa, mtu wa kwanza wakushirikiana naye ni mke wako kama umeoa, na ni mume wako kama umeolewa lakini, sio baba yako, sio mama yako.
Na wazazi wengine wasingetaka kuona kwamba unakuwa mbali nao kwa jinsi hii, wanataka waendeleze maamuzi yao na utawala wao waliokuwa nao juu yako mpaka kwenye ndoa yako, haiwezekani. Biblia inakataa. Sasa ukisoma ile Mwanzo unaweza ukafikiri ni wanaume tu wakioa ndio wanatakiwa watoke, waachane na wazazi wao, lakini Zaburi 45:10,11 inatuambia wazi kabisa, inasema, “Sikia, binti, utazame, utege sikio lako, Uwasahau watu wako na nyumba ya baba yako. Naye Mfalme atautamani uzuri wako, Maana ndiye bwana wako, nawe umsujudie”.
Sasa haimaanishi usiwasalimie, haimanishi usiwasaidie, lakini ningekuwa nazungumza kwa kiingereza ningekuambia, “your priorities must change” lazima ubadilike jinsi ambavyo unaweka kipaumbele katika watu ulio nao.
Unapoamua kuolewa, wa kwanza sio baba yako wala sio mama yako, wa kwanza ni mume wako baada ya Yesu. Katika mahusiano ya kibinadamu anayekuja pale wa kwanza baada ya Yesu moyoni mwako ni mume wako. Ikiwa hujafikia maamuzi ya namna hii moyoni mwako basi bado hujafikia utayari wa kuolewa. Na ina madhara yake magumu. Maana biblia inasema, kabla hujawasahau watu wako na watu wa nyumba ya baba yako, mume wako hawezi kuutamani uzuri wako, ukitaka autamani uzuri wako lazima uwasahau kwanza watu wa nyumbani kwa wazazi wako.
Sasa kuna tofauti ya kupenda na kutamani. Kabla hujaolewa au kabla hujaoa huruhusiwi kutamani. Lakini ukiisha oa unaruhusiwa kutamani lakini mke wako tu. Ukiishaoa kutamani mke wako ruksa, na biblia imeweka vizuri kabisa, na ukiishaolewa kutamani mume wako ni ruksa. Lakini biblia imeweka utaratibu wa ajabu sana kwamba, ili mume amtamani mke wake, lazima mke wake awasahau kwanza watu wa nyumbani mwa wazazi wake. Hiki ni kigezo kigumu sana.
Ndio maana unaweza ukakuta mtu ana mke mzuri sana lakini hamtamani. Unaweza ukafikiri labda ni kwa kuwa hajajipamba vizuri; lakini hata kama atajipamba, atajikwatua kuanzia asubuhi mpaka jioni, - anaweza hata akatumia muda mwingi kwenye kioo kuliko kwenye maombi akijitengeneza, lakini bado mume wake asimtamani; kwa nini? Kwa sababu ndani yake hajaachia watu wa nyumba ya wazazi wake. Au watu wa nyumba ya baba yake wana nafasi kubwa moyoni kuliko mume wake.
Ni mabadiliko ambayo lazima uyatarajie, watu wengi sana huwa hawafikirii hayo, wanafikiri ni kitu rahisi. Unaweza sasa ukaelewa kwa nini watu wengine ikifika siku ile ya “send off”, yaani ya kum’send’ msichana ‘off’ asikae tena nyumbani kwa baba yake, hiyo siku ni ngumu sana kwa wazazi. Kwa sababu wanajua, wanaagana na msichana wao, mahusiano yao waliokuwa nayo toka mwanzoni, tangu alipozaliwa, alipokuwa tumboni mpaka wakati huo yanabadilishwa, yanajengwa mengine, sasa anakwenda kuwa mke wa mtu, hawawezi tena kuingilia maamuzi juu yake, amefunga agano mahali pengine.
Unakuta siku hiyo wazazi wengine wanalia, unakuta vijana wengine wanalia, wasichana wengine wanalia. Usije ukafikiri ni kitu rahisi. Ndani ya nafsi kuna vitu vinaachana, kati ya wazazi na wale watoto wanaoana.
Mwl. C.Mwakasege