HONGERA KWA KUOKOKA
UTANGULIZI
Karibu kwenye Ufalme wa Mungu
Kitabu hiki kimeandikwa kwa ajili yako. Roho Mtakatikfu amekiweka mikononi mwako kwa kusudi muhimu la Mungu ndani ya Kristo.
Katika Jina lile lipitalo majina yote jina la Yesu Kristo, Bwana na Mwokozi wetu, napenda kukukaribisha katika Ufalme wa Mungu!
Imeandikwa wazi kabisa katika kitabu cha Waefeso 2:19 ya kuwa; “Basi tangu sasa ninyi si wageni wala wapitaji, bali ninyi ni wenyeji pamoja na watakatifu, watu wa nyumbani mwake Mungu”.
Umepata neema hii ya Mungu, na sasa umeokoka – biblia inakuambia tangu sasa wewe si mgeni wala mpitaji katika Ufalme wa Mungu - bali wewe ni mwenyeji pamoja na watakatifu wengi waliomo katika nyumba ya Mungu!
Nia ya Roho Mtakatifu kukuwekea kitabu hiki mikononi mwako, ni kukufahamisha angalau kwa kiasi fulani juu ya uamuzi uliofanya wa kutubu dhambi zako, na kumpokea Yesu Kristo kama Bwana na Mwokozi wako.
Kitabu hiki kitakusaidia kujua kitu gani kimetokea ulipookoka na mambo muhimu ya kufanya katika maisha hayo mapya ya wokovu.
Umefanya uamuzi wa busara – katika Luka 15:10 biblia inatuambia ya kuwa hata malaika wa mbinguni wanashangilia na kuufurahia uamuzi huo uliofanya.
Na mimi kama mtumishi wa Mungu aliye hai napenda kumshukuru Mungu katika Kristo Yesu kwa kukufunulia siri hii ya wokovu ambayo wengi hawajaiona na wengine wameiona lakini wanaipuzia. Ni maombi yangu kwa Mungu ya kuwa atakutia nguvu na kukupa ufahamu wa rohoni unapokisoma kitabu hiki ili kikusaidie katika maisha yako ya kila siku.


Christopher na Diana Mwakasege ,
S.L.P. 2166,
ARUSHA