Universal Chastity Education (UCE) – Tanzania
P. O. Box 86, Iringa. Email: ucetanzania@yahoo.com
Tel: (026) 2700585; Phone: 0713 778 808 / 0783 822 725
UCE - Helping People Live Healthy Lives


Universal Chastity Education (UCE) ni shirika lisilo la kiserikali lililosajiliwa chini ya Wizara ya Mambo ya Ndani Tanzania, mwezi wa pili mwaka 2009 kwa namba ya usajili SA 16196. Lengo kuu ni likiwa ni “Kuwasaidia Watu Waishi Maisha Yenye Afya”.

Dira ya UCE
“Kuwawezesha vijana ambao hawajaoa au kuolewa, kusubiri kwa kutoshiriki ngono kabla ya ndoa”.

Dhima ya UCE
“Kuwaelimisha vijana kuhusu kusubiri kwa kuzingatia taarifa, ufahamu, ujuzi na rasilimali sahihi ili waishi maisha yenye subira katika maswala ya ngono.

 Malengo ya UCE
1.      Kuwatia moyo vijana kusubiri kwa kutofanya ngono mpaka watakapooa au kuolewa na kuwa waaminifu ndani ya ndoa zao.
2.      Kuwatia moyo vijana kusubiri ili kuepukana na mimba zisizotarajiwa na magonjwa ya zinaa.
3.      Kushirikiana na mashirika / taasisi za serikali na zisizo za kiserikali, ndani na nje ya nchi kwa kuhamasisha vijana kusubiri na wanandoa kuwa waaminifu katika ndoa zao.
4.      Kutoa ushauri kwa vijana.
5.      Kuwahamasisha na kuwasaidia vijana kuona umuhimu wa maisha ya kifamilia mapema katika maisha yao.
6.      Kuhamasisha mabadiliko ya kitabia miongoni mwa vijana kwa kuhimiza vijana kuweka malengo, na kufanya maamuzi yenye tija na kulinda utu wao kimwili, kisaikolojia na kijamii.
7.      Kuwasaidia vijana kutafuta vyanzo vya taarifa muhimu na zenye maendeleo katika upeo mkubwa.

UCE tunaamini kwamba “KUSUBIRI NA KUWA MWAMINIFU NDANI YA NDOA” ndiyo njia pekee na iliyo sahihi katika kupunguza maambukizi ya virusi vya UKIMWI, mimba zisizotarajiwa, magonjwa ya zinaa, na matatizo ya kisaikolojia, kijamii na kimwili yatokanayo na ngono kabla na nje ya ndoa.

UCE hutoa elimu katika shule za sekondari, vyuoni na katika vikundi mbalimbali. Masomo yanayofundishwa ni pamoja na sababu zinazopelekea vijana kufanya ngono, kwa nini kusubiri,  upendo wa kweli huwa na subira (True Love Waits), kuweka malengo, kufanya maamuzi, kujitambua, kushi maisha yenye afya na kadhalika.

Chini ya UCE ipo huduma ya ushauri (counseling) wa mtu binafsi, kikundi, familia au wanandoa; watoto, vijana au watu wazima, katika matatizo ya kisaikolojia, kijamii, kiuchumi, kielimu, kifamilia, mahusiano, migogoro/ugomvi, pombe/madawa ya kulevya, matatizo ya kikazi, na kadhalika. Ushauri huu hutolewa na wataalamu wa ushauri kwa kuzingatia miiko na maadili ya taaluma yao.

Mipango
Mipango ya UCE imegawanyika katika vipengele vitatu. Kwanza tunatembelea shule na kutoa elimu kwa vijana / wanafunzi ikilenga umuhimu wa kusubiri na kutofanya ngono. Tukimaliza kutoa elimu tunagawa karatasi kwa kila mwanafunzi kuandika swali lake. Kulingana na muda tulionao tunajibu maswali na kwa yale tusiyoweza kuyajibu pale tunayaandika na kuyarejesha majibu. Baada ya maswali na majibu, wanafunzi walio tayari kusaini kadi kama ishara ya kudhibitisha maamuzi yao wanapatiwa kadi za kusaini.

Kipengele cha pili UCE tunaandaa semina kwa lengo la kuwajengea uwezo vijana waliosaini kadi. Semina hizi hufanyika kwa siku moja au mbili ambapo wanafunzi hupata nafasi ya kujifunza changamoto katika kusubiri na jinsi ya kusonga mbele katika kusubiri. Katika semina hizi huduma ya ushauri hutolewa kwa mwanafunzi mmoja mmoja au kikundi. UCE hugharamia semina hizi ikiwa pamoja na gharama za usafiri na chakula cha siku hiyo.

Kipengele cha tatu ni uanzishwaji wa klabu katika shule za sekondari. Klabu hizi hutoa mwanya wa kuendelea kujifunza na kupata msaada wa karibu wa ushauri. Ndani ya klabu tunaandaa waelimishaji rika.

Mipango ambatanishi ni pamoja na uandishi wa vitabu. Tumeandaa vitabu viwili
  1. “Kujamiiana Kabla, Wakati na Nje ya Ndoa” Ó 2011 kwa lengo la kuzungumzia kuhusu kujamiiana kwa uwazi na upana wake ili kujua nafasi yake katika maisha, na mahusiano baina ya mwanaume na mwanamke (tumechapa nakala 2000).




  1. “Pendo na Mahusiano” Ó 2012 lengo likiwa kuongeza wigo na upeo wa vijana katika kuelewa maana ya pendo, kujua undani wa pendo na kutoa mwanga wa utatuzi wa matatizo ya mahusiano kwa kuzingatia pendo la kweli huwa na subira  (tumechapa nakala 2000).




Rasilimali Watu
Timu ya UCE imeundwa na watu wanne ambao wamejitolea na sio kuajiriwa. Kila mwaka tunapokea wanafunzi wa mazoezi ambao nao husaidia katika kutoa huduma za ushauri kwa wanafunzi chini ya usimamizi wa timu ya UCE ambao nao ni washauri wenye taaluma ya ushauri.

Mafanikio
Tumefikia jumla ya shule za sekondari 85, vyuo 6 na mikutano ya vijana 10. Jumla ya watu 30,000 wamefikiwa na ujumbe wa UCE ambapo vijana 25583, wanaume 11217 na wanawake 14366 wameamua kusubiri na kusaini kadi kama ishara ya ahadi yao. N.B ( Takwimu za 2013)

Tumeona mabadiliko juu ya tabia ambapo wanafunzi wamejitambua na kufanya maamuzi ya kusubiri. Wengi wameelewa umuhimu wa kujiwekea malengo na kuyatimiza. Kupitia huduma ya ushauri wanafunzi wamepata nafasi ya kuelezea shida zinazowakabili katika maswala ya ngono na kupatiwa msaada na tiba kwa matatizo mbalimbali ya kisaikolojia.

Kwa mawasiliano piga: 0713 778 808