TAMKO LA JUKWAA LA WAKRISTO KUHUSU MAHAKAMA YA KADHI

JUKWAA LA WAKRISTO TANZANIA

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

image1

TAMKO LA JUKWAA LA WAKRISTO TANZANIA KUHUSU MUSWADA WA MAREKEBISHO YA SHERIA MBALIMBALI WA MWAKA 2014

Sisi Maaskofu, wajumbe wa jukwaa la Wakristo Tanzania, tuliokutana tarehe 20 Januari 2015, Dar es salaam, tumepata fursa ya kutafakari, kujadili na kujielimisha kwa kina yaliyomo katika Muswada wa Marekebisho ya Sheria Mbalimbali ya 2014 unaopendekeza, pamoja na mambo mengine, marekebisho ya Sheria ya Tamko la Sheria za Kiislamu la mwaka 1964. Mswaada huu unapendekeza kuanzishwa kwa Mahakama ya Kadhi. Baada ya mjadala wa kina tunatoa maoni yetu kama ifuatavyo: Mapendekezo ya kurekebisha Sheria ya Tamko la Sheria za Kiislamu ni mapendekezo makubwa yatakayokuwa na athari kubwa na nzito; kwani yanahoji msingi wa dola ya Tanzania kama dola isiyokuwa ya kidini. Kwa sababu hiyo, mapendekezo hayo yanaibua mambo mazito ya kikatiba ambayo hayawezi kuamuliwa na Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria Mbalimbali. Kama ambavyo tumesema mara nyingi, masuala yanayohusu imani za dini na kujiingiza kwa Serikali katika masuala yanayohusu imani hizo yanahitaji mjadala mpana na maridhiano ya kitaifa. Kwanza, Muswada huu unapendekeza kuanzisha Mahakama za Kadhi, licha ya sababu na madhumuni ya Muswada kusema kuwa lengo ni kutambua mahakama hizo. Kwa utaratibu wa sasa wa kisheria, Mahakama za Kadhi hazipo. Kwa hiyo, hoja ya kutambua uwepo wa mahakama hizo si sahihi. Kama inavyofahamika, Mahakama za Kadhi, pamoja na Mahakama za Wenyeji (Native Courts), zilizokuwepo wakati wa ukoloni zilifutwa na Sheria ya Mahakama za Mahakimu (Magistrates Courts Act) ya mwaka 1963. Tangu wakati huo,mahakama hizi hazipo na hazitambuliwi na sheria yoyote. Hivyo, mapendekezo ya Muswada huu yakipitishwa ndiyo yatazianzisha. Pili, kwa mapendekezo haya, Serikali inachukua jukumu la kuanzisha yenyewe taasisi za kidini kinyume na utaratibu wa kikatiba ambapo Serikali imekuwa haijishughulishi na uanzishwaji na uendeshaji wa taasisi za kidini. Hii ni kwa sababu Sheria ya Tamko la Sheria za Kiislamu haikuanzisha mahakama au taasisi nyingine yoyote ya kusimamia Sheria hiyo bali iliweka utaratibu wa mahakama za kawaida kuitambua na kuisimamia Sheria hiyo. Tatu, mapendekezo haya yanampa Waziri (ambaye ni kiongozi wa Serikali) mamlaka ya kutunga kanuni za utekelezaji wa maamuzi, hukumu na amri za Mahakama za Kadhi. Maana yake ni kwamba dola ya Tanzania, sio tu inakusudia kuanzisha mahakama ya kidini, bali pia kuweka utaratibu wa kutekeleza maamuzi, hukumu na amri za mahakama hizo. Nne, mapendekezo haya yanafuta utaratibu ambao umekuwepo kwa zaidi ya miaka hamsini ambao unatambua matumizi ya sheria za dini zisizokuwa za Kikristo katika masuala ya hadhi ya mtu, mirathi, ndoa na talaka kwa mujibu wa Sheria ya Ndoa, Mirathi na Talaka (Waasia wasio Wakristo), yaani “The Marriage, Succession and Divorce (Non- Christian Asiatics) Ordinance, Cap. 112”. Chini ya utaratibu huo, mila na desturi za watu wa imani zisizokuwa za Kikristo, mfano Wabahai, Wabudha, Wahindu, Khoja, n.k, zilikuwa zinatambuliwa kisheria. Chini ya mapendekezo ya Muswada huu, mila na desturi hizo zinafutwa na kunaingizwa utaratibu utakaotambua na kusimamia masuala na maslahi ya Waislamu peke yao. Ni wazi kuwa utaratibu unaopendekezwa ni wa kibaguzi na kinyume na matakwa/masharti ya Katiba ya sasa. Tano, kwa mapendekezo ya Muswada huu, hatuna hakika kama mamlaka za mahakama za sasa za kusikiliza na kuamua masuala ya hadhi ya mtu, mirathi na ndoa kwa mujibu wa Sheria ya Tamko la Sheria za Kiislamu itaendelea kuwepo. Aidha mapendekezo ya Muswada huu yako kimya juu ya uhusiano wa Mahakama za Kadhi na mahakama za kawaida. Kwa mfano, haieleweki (haikuwekwa wazi) kama kutakuwa na utaratibu wa rufaa, marejeo na mapitio ya maamuzi ya mahakama hizo. Endapo, kwa mfano, mtu hataridhika na maamuzi ya Mahakama ya Kadhi, je, atakuwa na haki ya kukata rufaa? Kama atakuwa na haki hiyo, rufaa hiyo itapelekwa kwenye mahakama au chombo gani? Sita, mapendekezo hayo hayo, pamoja na kwamba wadaawa wataenda kwa hiari yao, yako kimya juu ya kesi zinazohusu Waislamu na watu wa imani nyingine. Na hata kwa wadaawa ambao ni Waislamu, ikiwa upande mmoja (tuseme wa Mdai) unakwenda kwa hiari ila upande mwingine (wa Mdaiwa) unataka shauri lisikilizwe na mahakama ya kawaida, Muswada hautoi jibu nini kifanyike. Saba, kwa ufahamu wetu, baadhi ya madhehebu na taasisi za Kiislamu hazikubaliani na mamlaka ya Mufti kwenye masuala yao. Hivyo, kumpa Mufti mamlaka ya kutunga kanuni zitakazotumika katika Mahakama za Kadhi na kuwateua makadhi wenyewe kunaweza kusababisha migongano na migogoro ndani ya jamii za Waislamu. Nane, haturidhiki na hoja kwamba mahakama hizi hazitatumia fedha za umma. Kwa mfano, Waziri atakapokuwa anatunga kanuni atatumia fedha na rasilimali mbalimbali za umma. Vile vile, utekelezaji wa amri na hukumu za mahakama hizi utahitaji polisi na madalali wa mahakama ambao wanalipwa kwa fedha za umma. Tunatambua kwamba suala la Mahakama ya Kadhi lilikataliwa na Bunge Maalumu wakati wa kupitishwa kwa Katiba Inayopendekezwa. Tunaelewa kwamba hiyo Katiba Inayopendekezwa imetamka wazi kuwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni nchi “… isiyofungamana na dini yoyote….” Aidha, Katiba hiyo imetamka wazi kuwa “shughuli ya uendeshaji wa jumuiya za dini itakuwa nje ya shughuli za mamlaka ya serikali”. Hivyo, tunashangazwa na kufadhaishwa na suala hili kuibuka kwenye Muswada huu baada ya kuwa limekataliwa kwa namna hii na Bunge Maalumu. Kwa sababu zote hizo hapo juu, sisi viongozi wa Makanisa wanachama wa Jukwaa la Wakristo Tanzania tunaamini kwamba sababu zilizopelekea kufutwa kwa mahakama hizi mwaka 1963; yaani, kujenga umoja wa kitaifa, kuondoa ubaguzi katika mfumo wa kisheria na utoaji haki sawa, bado ni halali na za msingi leo hii. Kwa sababu hiyo, kwa heshima kubwa, tunashaurikwamba Serikali iondoe Muswada huu Bungeni ili kuepusha kuvunja misingi ya Taifa hili kama taifa lisilo la kibaguzi na lisilo fungamana na diniimage2